Coca-Cola ni moja ya kampuni maarufu duniani, ambayo hutengenezwa soda maarufu ya Coke na vinywaji vingine vya soda. Lakini, ilikuwaje hadi ikawa na jina hilo?
Labda umewahi kusikia kwamba Coca-Cola wakati mmoja ilikuwa na kiungo cha kusisimua ambacho kiliwafanya wateja kulipenda sana. Hii ni moja ya vilivyochangia jina lake.
“Coca”, kwa Kiswahili koka, ni jina la jani la mmea wa koka, moja ya viungo ambavyo mvumbuzi wa kinywaji hicho, mwanakemia wa Atlanta John Stith Pemberton, alichanganya na shira kutengeneza kinywaji chake.
Majani ya koka hutumiwa kutengeneza kokeini.
Wakati huo, mwishoni mwa karne ya 19, ilikuwa kawaida kwa majani ya koka kuchanganywa na divai na kuwa kinywaji cha kuchangamsha mwili.
Kinywaji kipya alichotengeneza Pemberton kilikuwa njia nzuri ya kukwepa sheria zilizoharamisha uuzwaji wa pombe.
Sehemu hiyo nyingine ya jina Coca-Cola inatokana na kiungo kingine chenye nguvu, ingawa si maarufu sana.
Kiungo hiki ni kola.
Ganda ambalo huwa na kokwa za kola ndani yake huwa na urefu wa inchi mbili na kabla ya kukauka, huwa za rangi ya kijani.
Ndani yake huwa na sehemu yenye fundo za rangi nyekundu au nyeupe kabla hazijakauka.
Asili ya kola ni Afrika Magharibi na zimekuwa zikitafunwa kwa miaka mingi na wenyeji kama kitu cha kuchangamsha mwili.
Kokwa hicho huwa na kafeini na theobromine, ambavyo hupatikana pia kwenye chai, kahawa na kakao. Zina pia sukari na kolanin, ambayo huaminika kuwa kichangamsha moyo.
Kufikia karne ya 19, kola zilianza kusafirishwa Ulaya na Marekani na zikaanza kutumiwa katika tembe zilizokusudiwa kutumiwa kuongeza nguvu mwilini.
Muda si muda, zilianza kutumiwa kwenye vinywaji. Kinywaji kimoja maarufu kilikuwa Vin Mariani, cha Ufaransa kilichotayarishwa kwa kuchanganya maji ya coca na divai nyekundu.
Kilitengenezwa na mwanakemia Mfaransa Angelo Mariani, mwaka 1863, na Papa Leo XIII alikuwa mmoja wa waliokipenda sana.
Malkia Victoria wa Uingereza, Thomas Edison, na Arthur Conan Doyle pia walikipenda sana.
Pemberton, naye alijitokeza na mchanganyiko wake akifuata mtindo huu lakini yeye hakutumia divai bali alitumia shira.
Baada ya muda kokeini iliacha kutumiwa kwenye vinywaji, baada ya kutambuliwa kama dawa ya kulevya lakini kola ziliendelea kuwa maarufu.
Kwa sasa, viungo pamoja na utaratibu wa kutayarisha soda za Coca-Cola huwa siri kuu, lakini taarifa husema huwa kola hazitumiwi tena. Badala yake, kampuni hiyo hutumia kemikali kuunda ladha sawa na ya kola.
Hata hivyo, jina halijabadilika.
Inakadiriwa kwamba chupa 1.9 bilioni za Coke huuzwa kila siku.
BBC
http://www.bbc.com/swahili/habari-37544715