Учебные тексты на суахили 5: Kwa nini wanawake India wanazikataa chale

Nchini India, na katika maeneo mengi duniani, kuchanjwa au kuchorwa chale ambazo hufahamika zaidi kama ‘tattoo’ hutazamwa kama ishara ya uhuru au kuasi.
Vijana wengi wanachanjwa chale kuonyesha utambulisho wao, jambo ambalo linawatambulisha kwa njia ya kipekee – sifa zao halisi.
Lakini kwa Geeta Pandey, uamuzi wake wa kupata chale ulikuwa aina yake ya kuasi, njia yake ya kudhihirisha uhuru wake aliokuwa ameupigania sana.
Ilikuwa njia yake ya kusema: “Sitafuata kanuni zilizowekwa.”
Anasema alikua akifikiria kwamba chale, pamoja na kutogwa kwenye sikio au pua, zilikuwa njia za kuwadunisha wanawake.
Hilo ni kwa sababu mamake alikuwa na chale kadha.
Na bibi yake alikuwa na hata zaidi.
“Na waliniambia kwamba hawakuwa na usemu kuhusu hayo,” anasema.
Katika jamii nyingi maeneo ya mashambani katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa India, anakotoka Pandey, ni lazima kwa wanawake ambao wameolewa kuwa na chale, ambazo kwa lugha yao hufahamika kama Godna.
“Familia yangu iliniambia kwamba iwapo singechanjwa chale, hakuna mtu hata mmoja kwenye familia hiyo ambayo angekunywa maji au kula chakula nilichokiandaa. Ningechukuliwa kuwa mtu mwenye uchafu, najisi, na asiyefaa kuguswa,” mamake Pandey anasema mamake alimwambia.
“Babangu bila shaka hakuhitajika kutogwa au kuwa na chale kwa sababu, alikuwa mvulana.”
Mamake aliozwa akiwa mtoto. Hakuna ametimiza miaka 11 wakati wa harusi yake miaka ya 1940.
Wiki chache baada ya sherehe hiyo, mwanamke mkongwe kutoka kijiji chake alifika nyumbani kwao kumchanja chale.

Historia ya chale

* Binadamu wamekuwa wakichanjwa chale kwa maelfu ya miaka.
* Zilitumiwa kuwatambua wafungwa, watumishi, vijakazi na watumwa.
* Wagiriki na Warumi enzi za kale walikuwa na chale, India pia.
* Wayahudi walichorwa chale zenye nambari za utambulisho walipokuwa wanazuiliwa na kufanyikwa kazi na Wanazi waliokuwa wanatawala Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
* Zilitumiwa pia kuwatambua binadamu na watu wa tabaka mbalimbali.
* Mara nyingi chale zilikuwa kama adhabu, na zilichukuliwa kama jambo la aibu au ishara ya kudunishwa.
* Wakati mwingine, zilikuwa ishara ya kumilikiwa na mtu fulani – mfano chale yenye nembo au alama ya baba wa mtu au mume wa mtu.

Vifaa alivyotumia vilikuwa vya msingi sana: sindano na moto.
Mchakato wote ulihusisha kuchomwa kwa sehemu ya juu ya ngozi na kujaza rangi kwenye chale.
Nyakati hizo, hakukuwa na dawa za kupunguza maumivu au mafuta ya kuharakisha shughuli ya kupona.
Chale wakati huo zilichukua mwezi mzima kupona.
Zaidi ya miaka sabini baadaye, chale za mamake Pandey karibu zimefutika, lakini bado anaukumbuka uchungu alioupitia.
“Nililia sana. Nilikuwa nampiga mateke mwanamke huyo aliyekuwa ananichanja. Mwishowe, alienda na kulalamika kwa babu yangu. Alisema mimi ni msumbufu,” mamake Pandey anasema.
Hajui chale alizochorwa zina maana gani na mwanawe Pandey haelewi pia.
“Labda pamechorwa phool-patti,” anasema, maana yake maua na majani.
Keya Pandey, mwanaathropojia wa kijamii kwa sasa katika chuo kikuu cha Lucknow ambaye amefanya utafiti sana kuhusu chale katika maeneo ya mashambani India anasema michoro mingi huwa na maua na majani ya mimea mbalimbali.
Kadhalika, wengine huchanjwa chale za majina ya waume zao au baba zao.
Kuna wengine huchorwa majina ya vijiji vyao au nembo za ukoo au ishara nyingine za kitamaduni, bila kusahau pia miungu.
Bi Pandey anasema ameona chale katika karibu kila jamii India na anakadiria kwamba mamilioni ya wanawake wana chale.
Katika baadhi ya jamii, hasa makabila ambayo yameendelea kudumisha utamaduni, wanawaume na wanawake huwa na chale.
“Ni ishara ya utambulisho, katika uhai na katika mauti. Wazo kwamba unapofariki roho yako husafiri mbinguni au jehanamu na utaulizwa ulikotoka, na hivyo unaweza kufahamu asili yako kupitia chale,” anasema Pandey.
Kuna jamii nyingine ambazo wanawake wake hupata chale kama mapambo.
Hata hivyo, kuna baadhi ya visa ambapo wanawake wa tabaka la chini walijichanja chale ili kuwafanya wasipodenze na hivyo kutowavutia wanaume wenye ushawishi ambao wakati mwingine wangewadhalilisha kimapenzi.
Lakini katika jamii nyingine, sana anakotoka Pandey, chale zilikuwa za wanawake pekee, ishara ya hali yake katika ndoa.
Kwa mamake na bibi yake, zilikuwa ishara ya kutakasika – kutokana na wazo kwamba iwapo mwanamke hangefanyiwa tambiko lenye uchungu hivyo, hangestahiki kukubalika katika jamii.
Utamaduni huo hata hivyo umeanza kufifia – na wanawake wengi na wasichana wanakataa kuchanjwa chale.
Maendeleo na maisha ya kisasa yameanza kubadili mtazamo wao na kadhalika mawasiliano na watu wengine kutoka nje ya vijiji vyao.
Utamaduni unaanza kubadilika na wasichana vijijini hawataki tena kupata chale.
Hilo linadhihirika zaidi miongoni mwa wasichana wa jamii ya Baiga.
Bi Pragya Gupta wa shirika la WaterAid India ambaye amezuru majuzi eneo la watu wa jamii ya Baiga kufahamu iwapo wana maji safi ya kunywa anasema wanawake wengi aliokutana nao wana chale.
Lakini wengi wa wasichana hawana.
Kuimarika kwa hali ya barabara, kuwepo kwa runinga na simu za rununu pia vimebadilisha mambo. Aidha, watoto wengi wanaenda shule na kubadili mtazamo wao kuhusu utamaduni huo.
“Nilikutana na Anita, 15. Ana chale usoni na aliniambia kwamba alihisi uchungu sana na kwamba hatachorwa chale nyingine. Mamake Badri, wa miaka 40, ana chale kote mwilini,” Bi Gupta anasema.
Uasi wa Anita unaungwa mkono na mamake.
“Nilikwua sijasoma na nilipokea niliyoambiwa na wazazi wangu bila kuuliza maswali. Lakini yeye huenda shuleni na hataki chale, hilo ni sawa kwangu,” anasema.
Miaka ya karibuni, raia wa India katika mitaa ya kifahari wameanza kupata chale pia, wakiiga waigizaji na wanamuziki nyota wa Hollywood.
Punder anasema marafiki zake wengi pia wana chale.
Lakini kwangu, kwa sababu ya utamaduni wangu, chale zinabaki mwiko – ishara ya kudunishwa kwa wanawake.

BBC Swahili
http://www.bbc.com/swahili/habari-41501207

Leave a Reply