Учебные тексты на суахили 2: Tafsiri nzuri na tafsiri mbovu

[Ёвин и Ива, не обращайте внимания. В Интернете не так просто найти хорошие тексты на суахили для учёбы, поэтому те, что мне попались, я буду складывать в блог]

Tafsiri ya neno kwa neno inadhoofisha maana – inaweza kupotosha maana ya kile kinachokusudiwa. Kwa hakika, kufasiri neno kwa neno huifanya tafsiri iwe mbovu.

Kila tafsiri ni fasiri au ufafanuzi wa maelezo fulani.

Sanaa ya kufasiri kwa Kiswahili si kazi rahisi kama wengi wanavyofikiri kwa sababu hakuna lugha iliyo sawa na Kiswahili.

Kazi ya kutafsiri maandishi kutoka lugha ya kigeni kwa Kiswahili inaweza kufanywa kwa urahisi na yeyote yule mwenye kamusi la maneno ya lugha hizo mbili.

Lakini fasiri yenye kutafsiri neno kwa neno sio tafsiri nzuri. Kwa hakika, si lazima kila neno lifasirike kwa neno moja. Maneno mengine huwa hayakubali kuamiliwa hivyo.

Mwenye kutafsiri anapoamua kutumia neno fulani badala ya jengine wakati huohuo anakuwa pia anachagua neno gani litalofuata ambalo atahitaji kulitumia.

Kwa hivyo uchaguzi wa neno ndio chanzo cha fasiri. Sauti pia, yaani namna neno linavyosikika husaidia kufikisha maana inayokusudiwa kwa wanaosikiliza au kusoma.

Tafsiri ya neno kwa neno inadhoofisha maana – inaweza kupotosha maana ya kile kinachokusudiwa. Kwa hakika, kufasiri neno kwa neno huifanya tafsiri iwe mbovu.

Tafsiri iliyo nzuri ni ile yenye kusema vilevile kama yasemavyo makala yaliyotafsiriwa, iwe inalingana na maandishi asili. Tafsiri iliyo nzuri huwa inaeleza mambo kana kwamba lugha iliyotumiwa ndio lugha asili iliyotumiwa kuandika makala hayo.

Tafsiri hiyo huwa na maana ya kinachokusudiwa katika maandishi yanayofasiriwa. Tafsiri aina hiyo huwa inatiririka kama maji; haikwami kwami.

Chaguo la neno moja linaweza kuamua mtiririko wa makala yote unayoyafasiri. Kutafsiri ni kazi ya hatua kwa hatua. Kwa hivyo, kumbuka kwamba unapoamua kutumia neno fulani katika hatua moja unaweza ukaiathiri hatua itayofuata hapo. Lakini kuchagua kutumia neno fulani na si jengine ni mwanzo tu.

Ni mwanzo kwa sababu tafsiri iliyo nzuri huwa pia inashikamana, sentensi moja inashikamana na nyingine, sehemu moja ya maelezo yanayofasiriwa inashikamana na nyingine.

Baadhi ya nyakati wafasiri wanaathiriwa na jinsi wafasiri wengine walivyotafsiri neno au mafungu ya maneno. Haya tunayaona wazi siku hizi katika matangazo ya redio au maandishi ya magazeti. Hatari hapa iko katika kuiga.

Kuna mifano mingi sana ya maneno yanayotafsiriwa vibaya na yanayoendelea kutumiwa na vyombo vya habari vya kuheshimika kwa sababu waandishi au watangazaji wamezoea kuigiza tafsiri zilizo mbovu.

Nitatoa hapa mifano miwili ya tafsiri mbovu. Zote zimetafsiri neno kwa neno na matokeo yake ni sentensi ambazo ingawa zina maneno ya Kiswahili hazisemi kama Waswahili tusemavyo.

1. “Waathiriwa wanapokea matibabu” ni tafsiri ya neno kwa neno ya sentensi ifuatayo ya Kiingereza: “The victims are receiving treatment.” Waswahili hatusemi kuwa “mgonjwa anapokea matibabu”. Tunasema kuwa “mgonjwa anatibiwa”.
2. “Je, unanipokea?” Hii ni tafsiri ya neno kwa neno ya sentensi ya Kiingereza: “Are you receiving me?” Mara nyingi tunawasikia watangazaji wakiisema sentensi hii wakiwa studio wakizungumza na ama waandishi wao au wahojiwa walio nje ya studio. Waswahili hatumuulizi mtu iwapo tunampokea. Tunamuuliza iwapo anatusikia. Lakini siku hizi kama nilivyosema watangazaji wamezoea kuwa “je, unanipokea?” badala ya “je, unasikia vizuri?”
Tafsiri nzuri haipatikani kwa uchawi. Inapatikana kwa juhudi za mwenye kufasiri za kuweza kuifanya tafsiri yake iwe na maana sawa na ile ya makala ya awali aliyoyafasiri.

Kuna jambo moja ambalo kila mwenye kufasiri anapaswa kulikumbuka. Nalo ni kwamba kazi ya kutafsiri kitu ni kazi ya usanii na si kazi ya sayansi. Hivyo, unaweza ukafasiri makala kwa uzuri utakiwavyo lakini bado anaweza akatokea mtu akaikosoa tafsiri yako.

Ni muhimu kwa hivyo kwamba usipoteze muda kubishana kuhusu, kwa mfano,namna ulivyozipanga sentensi zako. Lililo muhimu ambalo unapaswa ulizingatie ni iwapo tafsiri yako ina maana ileile kama iliyokusudiwa katika makala ya Kiingereza (au ya lugha yoyote nyingine) uliyoyafasiri.

Unapofasiri kitu usiwe na papara. Kuna hatari kwamba ukifanya pupa unaweza ukapotosha maana ya kinachokusudiwa. Soma kwa makini, mara mbili tatu ikiwezekana, hicho unachokitafsiri mpaka maana yake ikuingie sawasawa kichwani. Usianze kutafsiri chochote kabla ya kwanza kukielewa unachokifasiri. Halafu unapokuwa unafasiri ziangalie sentensi zako, au hata zisome kwa sauti, uangalie kama zinalingana na miundo ya sentensi za Kiswahili.

Jiulize pia iwapo fasiri yako ni sahihi na iwapo inafahamika vizuri. Haitoweza kufahamika iwapo utatumia miundo ya sentensi yenye kuigiza ile ya lugha ya Kiingereza (au lugha yoyote nyingine ya awali unayoifasiri).

Pia tafsiri yako haitoweza kufahamika ikiwa makala unayoyafasiri hayafahamiki. Kwa hivyo, usichelee kuwauliza wengine maana ya unachotaka kukitafsiri. Waombe wenzako wakueleze makala uliyo nayo yana maana gani au yanasema nini.

Tunapotafsiri huwa hatufasiri maneno tu bali huwa pia tunafasiri ada, kawaida, na utamaduni wa mila na hata wa kisiasa. Tunakuwa tunazishughulikia lugha mbili tafauti — au pingine zaidi ya mbili — na wakati huohuo tunakuwa pia tunashughulikia tamaduni mbili tafauti.

Kwa hivyo, jiepushe kutumia mifano kutoka tamaduni nyingine, jaribu uwezavyo kutumia mifano kutoka kwenye utamaduni wa Kiswahili.

Kwa hakika, inaweza kuwa kazi ngumu kutafsiri maneno ya kitamaduni. Tafauti baina ya tamaduni mbalimbali ni changamoto kubwa kwani tafauti hizo huenda zikampa matatizo mwenye kutafsiri kuliko tafauti za miundo ya lugha.

Kwa mfano, katika lugha yetu ya Kiswahili kuna maneno ambayo hatuyasemi waziwazi. Sehemu za utupu wa mwanadamu hatuziiti kwa majina yao. Ni muhali Waswahili kuziita sehemu hizo za utupu kwa majina yao. Lakini Waingereza hawana muhali huo. Wanayatumia katika mazungumzo na maandishi ya kawaida.

Hamna shaka yoyote ile kwamba kuyatafsiri maneno kama hayo kwa Kiswahili huwa ni kazi ngumu na huwatatiza baadhi ya wanaotafsiri.

Ugumu huo huenda ukawa ni kwa sababu ya tafauti baina ya tamaduni, dini, au imani. Kuna njia mbalimbali za kutafsiri maneno yenye muhali kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Tafsiri nzuri ni ile iliyo tiifu kwa makala ya chanzo, makala ya awali na pia inayowafanya watu wanaoisikiliza au kuisoma waikubali kwa namna makala yalivyotafsiriwa.

Tafauti baina ya tamaduni mbili zinaweza kuwafanya watu wa utamaduni mmoja waamini mambo, matukio au hata tabia ambazo watu wa utamaduni mwingine huenda wakaziona kuwa ni za ajabuajabu au za kuchekesha au hata zisizokubalika katika utamaduni wao.

Kila wakati mtafsiri anawajibika amfikiriye msikilizaji au msomaji wa makala au taarifa iliyotafsiriwa.

Kwa mfano ikiwa umetafsiri makala yatayotumiwa katika kipindi cha watoto cha redio au cha televisheni basi utalazimika uwe mwangalifu zaidi wa lugha utayoitumia ambayo itabidi iwe nyepesi.

BBC Academy
http://www.bbc.co.uk/academy/swahili/language/translation/article/art20131011115926129

Leave a Reply