Учебные тексты на суахили 3: Maneno mapya

Maneno mengi yanatungwa kwa sababu mahsusi na hukubalika kutumiwa na watu polepole baada ya muda mrefu.

Kawaida ya lugha ni kwamba hukua. Kukua kwake ni kwa kuongezeka kwa maneno yaliyo mapya au kwa maneno yaliyopo kuwa na maana mpya. Inasemekana kwamba lugha ya Kiingereza, kwa mfano, kila mwaka huongezeka maneno mapya yapatayo 20,000.

Hivyo ni sawa na kusema kwamba kila siku maneno mapya 55 yanaingia katika lugha hiyo. Kwa hesabu nyingine ni kwamba kila saa, mchana na usiku, maneno mapya mawili au matatu yanabuniwa katika lugha ya Kiingereza.

Kuna wenye kusema kwamba idadi hiyo ya maneno mapya ni ya kutia chumvi. Wengine wanasema kwamba kwa hakika idadi hiyo ni ndogo kuliko ilivyo hasa. Miongoni mwa maneno hayo mapya ni yale yanayohusika na sayansi, teknolojia pamoja na ya kibiashara.

Ingawa Kiswahili kinakua hata hivyo haielekei kwamba lugha hii inakua kwa kiwango kama hicho cha kuongezeka idadi kubwa hivyo ya maneno mapya.

Maneno mengi yanatungwa kwa sababu mahsusi na hukubalika kutumiwa na watu polepole baada ya muda mrefu. Ni taabu kung’amua ni lini hasa neno jipya linapoanza kukubalika kutumiwa. Idhaa ya Kiswahili ya BBC yenyewe ilikuwa zamani katika mstari wa mbele miongoni mwa waliokuwa wakitunga maneno mepya ya kutumiwa katika Kiswahili. Maneno kama ‘katiba’ na ‘kutaifisha’, kwa mfano, yalianza kwanza kutumiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC na polepole yakakubaliwa na kuanza kutumiwa na vyombo vingine vya habari vyinavyotumia lugha ya Kiswahili.

Neno ‘runinga’ lenye maana ya televisheni lilitungwa na Sheikh Ahmed Nabahany wa Kenya na sasa limekwishaanza kutumika na kukubalika.

Maneno mengine mepya katika lugha ya Kiswahili huanza kutumiwa na vijana barabarani mijini. Nchini Kenya, kwa mfano, baadhi ya maneno yanayotumiwa na vijana mitaani katika lugha yao ya ‘sheng’ huanza pia kutumiwa na wengine katika jamii na mwishowe hukubalika kuwa miongoni mwa msamiati halali wa Kiswahili.

Kwa hakika, katika miongo ya hivi karibuni lugha ya Kiswahili imekua sana kwa kuingizwa maneno mepya katika msamiati wake. Maneno hayo huwa ama yametungwa au yamebadilishwa kutoka lugha nyingine ili yalingane na Kiswahili au ‘yameazimwa’ kutoka lugha nyingine. Madhumuni ya maneno hayo mepya ni kuelezea dhana ambazo hazijakuwako katika ulimwengu wa Kiswahili.

Mengi ya maneno mepya yamebuniwa katika sayansi na teknolojia. Huo ni ushahidi ulio wazi kwamba Kiswahili bado hakijakomaa. Hata hivyo, juu ya kubuniwa maneno chungu nzima yaliyo mepya maneno hayo bado hayatumiwi na watu wa kawaida. Kama yanatumiwa basi hutumiwa na watu wachache tu walio wataalamu wa fani hizo.

Kuna maneno mengine ambayo hata hao wataalam hawayatumii kwani maneno hayo hubakia katika kumbukumbu za maktaba au za walioyabuni maneno hayo.

Dosari moja lililopo katika msamiati wa Kiswahili ni kwamba hata makamusi yanayosifika yanakosa baadhi ya maneno mepya (na hata ya kale) yanayotumiwa sana siku hizi na watu wa kawaida.

Katika miaka ya hivi karibuni kumetungwa makamusi kadhaa yenye kujaribu kukidhi haja ya kuyaeneza na kuyaeleza maneno mepya ya Kiswahili yanayohusika na mambo ya sayansi, tekinolojia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Mifano mizuri ni Kamusi ya Awali ya Sayansi na Tekinolojia na Kamusi ya Kemia, Fizikia na Biolojia.

Kwa hakika, kila chumba cha habari kinahitajika kiwe na makamusi kama hayo yenye kuelezea maana ya maneno ya kisayansi na ya kiteknolojia.

Tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kumepatikana maendeleo makubwa duniani katika nyanja za sayansi, ufundi, viwanda, sayansi ya jamii na utamaduni pamoja na elimu. Maendeleo hayo makubwa yamezusha haja ya kubuni msamiati mpya wa maneno yatayotumika katika nyanja hizo si katika lugha ya Kiswahili tu bali pia katika lugha nyinginezo, pamoja na ya Kiingereza.

Hivi sasa kuna dhana kwamba ulimwengu mzima ni ‘kijiji kimoja’ tu chenye mifumo ya hali ya juu ya kisiasa na kiuchumi kutokana na mapinduzi makubwa yaliotokea katika nyanja za usafiri na mawasiliano. Hivyo, maneno mepya yanayotumiwa katika lugha za kigeni, hasa ya Kiingereza, ni rahisi sana kupenya na kuingia katika msamiati wa Kiswahili. Maneno hayo zaidi huwa ni ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Ugumu wa kupata maneno ya Kiswahili yanayoweza kusibu kutumika katika nyanja hiyo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano umesababisha maneno ya Kiingereza yanayotumika katika nyanja hiyo yawe sasa yanatumika, bila ya kubadilishwa sana, katika lugha ya Kiswahili. Mifano iko mingi: folda (folder), kiibodi (keyboard), yuza nem (user name), kudelete (to delete), kusaaf au kubrauz (to surf, to browse), skrini (screen) na kontrol key (control key).

Jambo lililo muhimu ni kwamba tunapoanza kuyatumia maneno mepya yaliokubalika tuyatumie kwa njia ambayo itakuwa rahisi kwa msikilizaji au msomaji kuelewa unakusudia nini.

Maneno kama ‘tabia nchi’ na ‘utandawazi’ ingawa hayakuanza kutumika kwa muda mrefu sana hivi sasa yamekwishakuwa maneno ya kawaida yanayofahamika na wasikilizaji wa redio au televisheni au wasomaji wa magazeti na wa mablogi.

BBC Academy
http://www.bbc.co.uk/academy/swahili/language/new-words/article/art20131030124225972

Leave a Reply