Учебный текст на суахили 6: Wanandoa wanaotafuta vizazi vya kukopesha waelekea Ukraine

Ukraine, ni miongoni mwa mataifa masikini barani Ulaya, na limeanza kuwa kivutio kikubwa kwa wanandoa wanaotaka kubebewa mimba.Fedha zinazopewa wanawake wanaoshiriki katika mpango huo zinawavutia wanawake wengi, lakini pia kuna changamoto zake.
Ana alikuwa na miaka 18 wakati alipogundua kuhusu biashara ya kubeba mimba kupitia kwa runinga.
Alikuwa amemaliza shule ya upili na alikuwa na mpango wa kufanya kazi katika hoteli katika mji wa magharibi wa Ukrain ambapo watalii huzuru. Kazi hiyo hulipa $200 kwa mwezi, lakini kwa kumbebea mtu mwengine mimba aligundua anaweza kujipatia $20,000 (£14,000).
Familia ya Ana sio masikini kwa viwango vya kawaida. Mamake ni mhasibu na amekuwa akimsaidia kila mara.
Lakini anasema alivutiwa na biashara ya kubeba mimba, kwa kuwa alitaka kupata fedha ili kuweza kununua vitu vya ghali,kurekebisha nyumba, gari na mambo mengine.
Ijapokuwa mamia ya wanawake hushiriki katika biashara hiyo,mpango huo hauzungumziwi hadharani nchini Ukraine.
Wanandoa wa kigeni wamekuwa wakitembelea taifa hilo kwa wingi tangu 2015, wakati vituo vya kubeba mimba barani Asia vilipoanza kufunga viwanda vyao moja baada ya chengine, huku kukiwa na ripoti za unyanyasaji.
Huku wakizuiwa nchini India, Nepal na Thailand, waliamua kuelekea Ukraine ikiwa ni miongoni mwa maeneo machache ambayo yanaendelea na biashara hiyo pamoja na gharama kama ile ya Marekani.
”Tuna wanadoa wengi wasio na watoto wanaokuja katika taifa hili”, alisema Ana ambaye hakutaka kutambulishwa. Wakati alipokuwa na umri wa miaka 21 na baada ya miaka kadhaa ya kufanya kazi hotelini, Ana hatimaye alikubali kubeba mimba.
Wakati huo alikuwa na mtoto hatua iliomfanya kukubali.
Chini ya sheria ya Ukraine,mama atakayebeba mimba lazima awe na mtoto wake mwenyewe kabla ya kushiriki katika biashara ya kubeba mimba ya mtu mwengine.
Iwapo una mtoto wako mwenyewe hautakuwa na mapenzi mengi na mtoto uliombeba, kulingana na wale wanaowaajiri wanawake hao.
Ni safari ndefu.
Ana alianza kuutazama mtandao ambao wanawake wanaobeba mimba za biashara, maajenti, kliniki na wafanyibiashara wa biashara hiyo huweka matangazo yao.
Na muda mfupi baadaye alielekea katika mji mkuu wa Kiev yapata kilomita 450 ili kukaguliwa kiafya.
Aliandikisha kandarasi na wanadoa kutoka Slovenia waliokuwa na tatizo la kupata mtoto.
Ana alikuwa na bahati, kiinitete kiliwekwa katika kizazi chake na kuanza mpango wote wa kubeba mimba kwa minajili ya biashara. Lakini ni wakati huo ambapo changamoto zilianza, anasema.
Anasema kuwa huduma za kiafya wanazopewa ni za kiwango cha chini, wanawake wengine waliobeba mimba walikuwa na matatizo ya kiafya ambayo hayakuangaziwa ama hata kutibiwa kwa wakati na hivyobasi kuzua matatizo mengine, anasema.
Aliweka malalamishi yake katika mtandao wa kijamii ili kuwaonya wanawake wengine lakini alikemewa na kliniki hiyo na sasa bado anaogopa kuwataja hadharani.
Mtoto aliyejifungua alizaliwa akiwa na afya njema lakini mpango wote ulikuwa wa kuogofya.
Bado, amekubali kwa mare nyengine kubeba mimba nyengine wakati huu akiwabebea wanadoa wa Japan. wanafuatilia maswala yote kupitia wakili mmoja mjini Kiev na kuna uwezekano mkubwa kwamba hatokutana nao ana kwa ana.
Ana wakati huu amekuwa na makini katika kuchagua kliniki,lakini iwapo mpango wote utafanikiwa, kufikia miaka 24 atakuwa amejifungua watoto watatu, mmoja akiwa wake na wengine wawili wa mtu mwengine.
Ukiwa mji mkuu wa Biashara ya kubeba mimba
Mahitaji ya kubeba mimba kwa lengo la kupata malipo nchini Ukraine yamepanda kwa asilimia 1000 katika kipindi cha miaka 2 iliopita pekee, anasema Sam Everringham wa shirika la familia kupitia ubebaji mimba wa biashara, shirika la hisani nchini Sidney ambalo huwashauri wanaotarajiwa kuwa wazazi.
Taifa hilo anaongezea, limejipata kwa bahati mbaya miongoni mwa mataifa ambayo yanaruhusu utalii wa kubeba mimba za biashara.
Licha ya kwamba sheria hiyo ni halali nchini Ukraine inawatambua wazazi wanaotarajiwa kuwa wazazi kutoka wakati mimba inaposhika na haitoi kiwango cha mwisho cha fedha ambazo anayebeba mimba hiyo atalipwa -hatua inayowapatia fursa wanaobeba kunadi bei.
Lakini haimaanishi kwamba ni swala la moja kwa moja. Ikitegemea unakotoka, mkakati wa kumtoa mtoto huyo nje ya taoifa hilo inaweza kuwa ndoto kali huku wanandoa kutoka mataifa kadhaa ikiwemo Uingereza wakilazimika kusalia nchini humo kwa miezi kadhaa.
Huku kliniki nyingi nchini Ukraine zikionekana kufanya kazi kwa uwazi na kuwahudumia wanawake hao vizuri washirika wengi katika sekta hiyo pamoja na wanawake wanaobeba mimba hizo huzungumzia kuhusu wale walio na sifa mbaya.
Kuna ripoti kadhaa ambazo hazijathibitishwa kuhusu viinitete vinavyobadilishwa na ukaguzi wa kiafya wa viwango vya chini
“Kuna mifano ambapo maajenti wa UKraine wamekataa kulipa gharama za kubeba mimba iwapo mbebaji atakiuka miko mikali, iwapo ataavya mimba”, kulingana na bi Everingham.
Kuna mifano mibaya ambapo maajenti hubadilika na kuwa wanyama iwapo mpango wa kubeba mimba haukuwafurahisha wazazi.
Olga Bogomolets, daktari na mbunge ambaye anaongoza kamati ya bunge nchini Ukraine kuhusu afya anasema kuwa anaamini wanawake wadogo wanavutiwa na kubeba mimba za biashara kutokana na kuanguka kwa hali ya maisha katika taifa hilo.
Uchumi wa taifa hilo uliathiriwa na mfumuko mbaya 2014 na 2015 kutokana na mzozo unaoendelea mashariki mwa Ukraine kati ya jeshi na wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi.
Sekta hiyo kulingana na bi Bogomolets haijadhibitiwa vilivyo hivyobasi swala hilo linawaweka wabebabaji mimba na wazazi wanaolipa katika hatari
Wizara ya afya haijatoa tamko lolote kufuatia ombi la kutaka kufanya hivyo.
Tetiana anaishi na mamake lakini ameficha mimba alionayo akisema kuwa angependa kuelekea Kiev kutafuta kazi.Jana ambaye alijifungua mizezi miwli iliopita, anamshauri Tetiana anafaa kuchukulia biashara ya kubeba mimba kama kazi ya kawaida.
Anakumbuka mtoto aliyejifungua akichukuliwa mara tu alipojifungua huku akiwa amechoka katika kitanda chake.Anakiri kwamba hisia za kujifungua humjaa na alifikiria kuhusu mtoto huyo alipoelekea nyumbani.
Utakuwa mtu mbaya sana kutohisi hilo., anasema.lakini unapoona furaha na tabasamu kutoka kwa wazazi wenyewe, unagundua kwamba kila kitu kiko sawa na mtoto yuko katika hali nzuri.
Akiwa nyumbani na mwanawe magharibi mwa Ukraine, Ana pia anafikiria jukumu lake la kubeba mimba.Karibuni ataanza safari ya saa saba ya treni ili kuelekea kuelekea Kiev ili kuwekwa kiinitete katika kizazi chake.
Ijapokuwa ni hatua ngumu, ana matumaini ya kile atakachopata. Anataka kutumia fedha hizo kujinunulia jumba moja la ghorofa. Na pia anafurahia kile atakachowafanyia wazazi waliomlipa kuwabebea mimba.
”Wakati wanapobubujikwa na machozi ya furaha na kukushukuru, unahisi kitu ulichowafanyia”, anasema. Waliniambia kwamba mimi ni mtu muhimu sana katika maisha yao”.

Источник:
BBC Swahili
http://www.bbc.com/swahili/habari-43046665

Учебные тексты на суахили 5: Kwa nini wanawake India wanazikataa chale

Nchini India, na katika maeneo mengi duniani, kuchanjwa au kuchorwa chale ambazo hufahamika zaidi kama ‘tattoo’ hutazamwa kama ishara ya uhuru au kuasi.
Vijana wengi wanachanjwa chale kuonyesha utambulisho wao, jambo ambalo linawatambulisha kwa njia ya kipekee – sifa zao halisi.
Lakini kwa Geeta Pandey, uamuzi wake wa kupata chale ulikuwa aina yake ya kuasi, njia yake ya kudhihirisha uhuru wake aliokuwa ameupigania sana.
Ilikuwa njia yake ya kusema: “Sitafuata kanuni zilizowekwa.”
Anasema alikua akifikiria kwamba chale, pamoja na kutogwa kwenye sikio au pua, zilikuwa njia za kuwadunisha wanawake.
Hilo ni kwa sababu mamake alikuwa na chale kadha.
Na bibi yake alikuwa na hata zaidi.
“Na waliniambia kwamba hawakuwa na usemu kuhusu hayo,” anasema.
Katika jamii nyingi maeneo ya mashambani katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa India, anakotoka Pandey, ni lazima kwa wanawake ambao wameolewa kuwa na chale, ambazo kwa lugha yao hufahamika kama Godna.
“Familia yangu iliniambia kwamba iwapo singechanjwa chale, hakuna mtu hata mmoja kwenye familia hiyo ambayo angekunywa maji au kula chakula nilichokiandaa. Ningechukuliwa kuwa mtu mwenye uchafu, najisi, na asiyefaa kuguswa,” mamake Pandey anasema mamake alimwambia.
“Babangu bila shaka hakuhitajika kutogwa au kuwa na chale kwa sababu, alikuwa mvulana.”
Mamake aliozwa akiwa mtoto. Hakuna ametimiza miaka 11 wakati wa harusi yake miaka ya 1940.
Wiki chache baada ya sherehe hiyo, mwanamke mkongwe kutoka kijiji chake alifika nyumbani kwao kumchanja chale.

Historia ya chale

* Binadamu wamekuwa wakichanjwa chale kwa maelfu ya miaka.
* Zilitumiwa kuwatambua wafungwa, watumishi, vijakazi na watumwa.
* Wagiriki na Warumi enzi za kale walikuwa na chale, India pia.
* Wayahudi walichorwa chale zenye nambari za utambulisho walipokuwa wanazuiliwa na kufanyikwa kazi na Wanazi waliokuwa wanatawala Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
* Zilitumiwa pia kuwatambua binadamu na watu wa tabaka mbalimbali.
* Mara nyingi chale zilikuwa kama adhabu, na zilichukuliwa kama jambo la aibu au ishara ya kudunishwa.
* Wakati mwingine, zilikuwa ishara ya kumilikiwa na mtu fulani – mfano chale yenye nembo au alama ya baba wa mtu au mume wa mtu.

Vifaa alivyotumia vilikuwa vya msingi sana: sindano na moto.
Mchakato wote ulihusisha kuchomwa kwa sehemu ya juu ya ngozi na kujaza rangi kwenye chale.
Nyakati hizo, hakukuwa na dawa za kupunguza maumivu au mafuta ya kuharakisha shughuli ya kupona.
Chale wakati huo zilichukua mwezi mzima kupona.
Zaidi ya miaka sabini baadaye, chale za mamake Pandey karibu zimefutika, lakini bado anaukumbuka uchungu alioupitia.
“Nililia sana. Nilikuwa nampiga mateke mwanamke huyo aliyekuwa ananichanja. Mwishowe, alienda na kulalamika kwa babu yangu. Alisema mimi ni msumbufu,” mamake Pandey anasema.
Hajui chale alizochorwa zina maana gani na mwanawe Pandey haelewi pia.
“Labda pamechorwa phool-patti,” anasema, maana yake maua na majani.
Keya Pandey, mwanaathropojia wa kijamii kwa sasa katika chuo kikuu cha Lucknow ambaye amefanya utafiti sana kuhusu chale katika maeneo ya mashambani India anasema michoro mingi huwa na maua na majani ya mimea mbalimbali.
Kadhalika, wengine huchanjwa chale za majina ya waume zao au baba zao.
Kuna wengine huchorwa majina ya vijiji vyao au nembo za ukoo au ishara nyingine za kitamaduni, bila kusahau pia miungu.
Bi Pandey anasema ameona chale katika karibu kila jamii India na anakadiria kwamba mamilioni ya wanawake wana chale.
Katika baadhi ya jamii, hasa makabila ambayo yameendelea kudumisha utamaduni, wanawaume na wanawake huwa na chale.
“Ni ishara ya utambulisho, katika uhai na katika mauti. Wazo kwamba unapofariki roho yako husafiri mbinguni au jehanamu na utaulizwa ulikotoka, na hivyo unaweza kufahamu asili yako kupitia chale,” anasema Pandey.
Kuna jamii nyingine ambazo wanawake wake hupata chale kama mapambo.
Hata hivyo, kuna baadhi ya visa ambapo wanawake wa tabaka la chini walijichanja chale ili kuwafanya wasipodenze na hivyo kutowavutia wanaume wenye ushawishi ambao wakati mwingine wangewadhalilisha kimapenzi.
Lakini katika jamii nyingine, sana anakotoka Pandey, chale zilikuwa za wanawake pekee, ishara ya hali yake katika ndoa.
Kwa mamake na bibi yake, zilikuwa ishara ya kutakasika – kutokana na wazo kwamba iwapo mwanamke hangefanyiwa tambiko lenye uchungu hivyo, hangestahiki kukubalika katika jamii.
Utamaduni huo hata hivyo umeanza kufifia – na wanawake wengi na wasichana wanakataa kuchanjwa chale.
Maendeleo na maisha ya kisasa yameanza kubadili mtazamo wao na kadhalika mawasiliano na watu wengine kutoka nje ya vijiji vyao.
Utamaduni unaanza kubadilika na wasichana vijijini hawataki tena kupata chale.
Hilo linadhihirika zaidi miongoni mwa wasichana wa jamii ya Baiga.
Bi Pragya Gupta wa shirika la WaterAid India ambaye amezuru majuzi eneo la watu wa jamii ya Baiga kufahamu iwapo wana maji safi ya kunywa anasema wanawake wengi aliokutana nao wana chale.
Lakini wengi wa wasichana hawana.
Kuimarika kwa hali ya barabara, kuwepo kwa runinga na simu za rununu pia vimebadilisha mambo. Aidha, watoto wengi wanaenda shule na kubadili mtazamo wao kuhusu utamaduni huo.
“Nilikutana na Anita, 15. Ana chale usoni na aliniambia kwamba alihisi uchungu sana na kwamba hatachorwa chale nyingine. Mamake Badri, wa miaka 40, ana chale kote mwilini,” Bi Gupta anasema.
Uasi wa Anita unaungwa mkono na mamake.
“Nilikwua sijasoma na nilipokea niliyoambiwa na wazazi wangu bila kuuliza maswali. Lakini yeye huenda shuleni na hataki chale, hilo ni sawa kwangu,” anasema.
Miaka ya karibuni, raia wa India katika mitaa ya kifahari wameanza kupata chale pia, wakiiga waigizaji na wanamuziki nyota wa Hollywood.
Punder anasema marafiki zake wengi pia wana chale.
Lakini kwangu, kwa sababu ya utamaduni wangu, chale zinabaki mwiko – ishara ya kudunishwa kwa wanawake.

BBC Swahili
http://www.bbc.com/swahili/habari-41501207

Учебные тексты на суахили 4: Coca-Cola ilivyopata jina lake

Coca-Cola ni moja ya kampuni maarufu duniani, ambayo hutengenezwa soda maarufu ya Coke na vinywaji vingine vya soda. Lakini, ilikuwaje hadi ikawa na jina hilo?

Labda umewahi kusikia kwamba Coca-Cola wakati mmoja ilikuwa na kiungo cha kusisimua ambacho kiliwafanya wateja kulipenda sana. Hii ni moja ya vilivyochangia jina lake.
“Coca”, kwa Kiswahili koka, ni jina la jani la mmea wa koka, moja ya viungo ambavyo mvumbuzi wa kinywaji hicho, mwanakemia wa Atlanta John Stith Pemberton, alichanganya na shira kutengeneza kinywaji chake.
Majani ya koka hutumiwa kutengeneza kokeini.
Wakati huo, mwishoni mwa karne ya 19, ilikuwa kawaida kwa majani ya koka kuchanganywa na divai na kuwa kinywaji cha kuchangamsha mwili.
Kinywaji kipya alichotengeneza Pemberton kilikuwa njia nzuri ya kukwepa sheria zilizoharamisha uuzwaji wa pombe.
Sehemu hiyo nyingine ya jina Coca-Cola inatokana na kiungo kingine chenye nguvu, ingawa si maarufu sana.
Kiungo hiki ni kola.
Ganda ambalo huwa na kokwa za kola ndani yake huwa na urefu wa inchi mbili na kabla ya kukauka, huwa za rangi ya kijani.
Ndani yake huwa na sehemu yenye fundo za rangi nyekundu au nyeupe kabla hazijakauka.
Asili ya kola ni Afrika Magharibi na zimekuwa zikitafunwa kwa miaka mingi na wenyeji kama kitu cha kuchangamsha mwili.
Kokwa hicho huwa na kafeini na theobromine, ambavyo hupatikana pia kwenye chai, kahawa na kakao. Zina pia sukari na kolanin, ambayo huaminika kuwa kichangamsha moyo.
Kufikia karne ya 19, kola zilianza kusafirishwa Ulaya na Marekani na zikaanza kutumiwa katika tembe zilizokusudiwa kutumiwa kuongeza nguvu mwilini.
Muda si muda, zilianza kutumiwa kwenye vinywaji. Kinywaji kimoja maarufu kilikuwa Vin Mariani, cha Ufaransa kilichotayarishwa kwa kuchanganya maji ya coca na divai nyekundu.
Kilitengenezwa na mwanakemia Mfaransa Angelo Mariani, mwaka 1863, na Papa Leo XIII alikuwa mmoja wa waliokipenda sana.
Malkia Victoria wa Uingereza, Thomas Edison, na Arthur Conan Doyle pia walikipenda sana.
Pemberton, naye alijitokeza na mchanganyiko wake akifuata mtindo huu lakini yeye hakutumia divai bali alitumia shira.
Baada ya muda kokeini iliacha kutumiwa kwenye vinywaji, baada ya kutambuliwa kama dawa ya kulevya lakini kola ziliendelea kuwa maarufu.
Kwa sasa, viungo pamoja na utaratibu wa kutayarisha soda za Coca-Cola huwa siri kuu, lakini taarifa husema huwa kola hazitumiwi tena. Badala yake, kampuni hiyo hutumia kemikali kuunda ladha sawa na ya kola.
Hata hivyo, jina halijabadilika.
Inakadiriwa kwamba chupa 1.9 bilioni za Coke huuzwa kila siku.

BBC
http://www.bbc.com/swahili/habari-37544715

Учебные тексты на суахили 3: Maneno mapya

Maneno mengi yanatungwa kwa sababu mahsusi na hukubalika kutumiwa na watu polepole baada ya muda mrefu.

Kawaida ya lugha ni kwamba hukua. Kukua kwake ni kwa kuongezeka kwa maneno yaliyo mapya au kwa maneno yaliyopo kuwa na maana mpya. Inasemekana kwamba lugha ya Kiingereza, kwa mfano, kila mwaka huongezeka maneno mapya yapatayo 20,000.

Hivyo ni sawa na kusema kwamba kila siku maneno mapya 55 yanaingia katika lugha hiyo. Kwa hesabu nyingine ni kwamba kila saa, mchana na usiku, maneno mapya mawili au matatu yanabuniwa katika lugha ya Kiingereza.

Kuna wenye kusema kwamba idadi hiyo ya maneno mapya ni ya kutia chumvi. Wengine wanasema kwamba kwa hakika idadi hiyo ni ndogo kuliko ilivyo hasa. Miongoni mwa maneno hayo mapya ni yale yanayohusika na sayansi, teknolojia pamoja na ya kibiashara.

Ingawa Kiswahili kinakua hata hivyo haielekei kwamba lugha hii inakua kwa kiwango kama hicho cha kuongezeka idadi kubwa hivyo ya maneno mapya.

Maneno mengi yanatungwa kwa sababu mahsusi na hukubalika kutumiwa na watu polepole baada ya muda mrefu. Ni taabu kung’amua ni lini hasa neno jipya linapoanza kukubalika kutumiwa. Idhaa ya Kiswahili ya BBC yenyewe ilikuwa zamani katika mstari wa mbele miongoni mwa waliokuwa wakitunga maneno mepya ya kutumiwa katika Kiswahili. Maneno kama ‘katiba’ na ‘kutaifisha’, kwa mfano, yalianza kwanza kutumiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC na polepole yakakubaliwa na kuanza kutumiwa na vyombo vingine vya habari vyinavyotumia lugha ya Kiswahili.

Neno ‘runinga’ lenye maana ya televisheni lilitungwa na Sheikh Ahmed Nabahany wa Kenya na sasa limekwishaanza kutumika na kukubalika.

Maneno mengine mepya katika lugha ya Kiswahili huanza kutumiwa na vijana barabarani mijini. Nchini Kenya, kwa mfano, baadhi ya maneno yanayotumiwa na vijana mitaani katika lugha yao ya ‘sheng’ huanza pia kutumiwa na wengine katika jamii na mwishowe hukubalika kuwa miongoni mwa msamiati halali wa Kiswahili.

Kwa hakika, katika miongo ya hivi karibuni lugha ya Kiswahili imekua sana kwa kuingizwa maneno mepya katika msamiati wake. Maneno hayo huwa ama yametungwa au yamebadilishwa kutoka lugha nyingine ili yalingane na Kiswahili au ‘yameazimwa’ kutoka lugha nyingine. Madhumuni ya maneno hayo mepya ni kuelezea dhana ambazo hazijakuwako katika ulimwengu wa Kiswahili.

Mengi ya maneno mepya yamebuniwa katika sayansi na teknolojia. Huo ni ushahidi ulio wazi kwamba Kiswahili bado hakijakomaa. Hata hivyo, juu ya kubuniwa maneno chungu nzima yaliyo mepya maneno hayo bado hayatumiwi na watu wa kawaida. Kama yanatumiwa basi hutumiwa na watu wachache tu walio wataalamu wa fani hizo.

Kuna maneno mengine ambayo hata hao wataalam hawayatumii kwani maneno hayo hubakia katika kumbukumbu za maktaba au za walioyabuni maneno hayo.

Dosari moja lililopo katika msamiati wa Kiswahili ni kwamba hata makamusi yanayosifika yanakosa baadhi ya maneno mepya (na hata ya kale) yanayotumiwa sana siku hizi na watu wa kawaida.

Katika miaka ya hivi karibuni kumetungwa makamusi kadhaa yenye kujaribu kukidhi haja ya kuyaeneza na kuyaeleza maneno mepya ya Kiswahili yanayohusika na mambo ya sayansi, tekinolojia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Mifano mizuri ni Kamusi ya Awali ya Sayansi na Tekinolojia na Kamusi ya Kemia, Fizikia na Biolojia.

Kwa hakika, kila chumba cha habari kinahitajika kiwe na makamusi kama hayo yenye kuelezea maana ya maneno ya kisayansi na ya kiteknolojia.

Tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kumepatikana maendeleo makubwa duniani katika nyanja za sayansi, ufundi, viwanda, sayansi ya jamii na utamaduni pamoja na elimu. Maendeleo hayo makubwa yamezusha haja ya kubuni msamiati mpya wa maneno yatayotumika katika nyanja hizo si katika lugha ya Kiswahili tu bali pia katika lugha nyinginezo, pamoja na ya Kiingereza.

Hivi sasa kuna dhana kwamba ulimwengu mzima ni ‘kijiji kimoja’ tu chenye mifumo ya hali ya juu ya kisiasa na kiuchumi kutokana na mapinduzi makubwa yaliotokea katika nyanja za usafiri na mawasiliano. Hivyo, maneno mepya yanayotumiwa katika lugha za kigeni, hasa ya Kiingereza, ni rahisi sana kupenya na kuingia katika msamiati wa Kiswahili. Maneno hayo zaidi huwa ni ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Ugumu wa kupata maneno ya Kiswahili yanayoweza kusibu kutumika katika nyanja hiyo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano umesababisha maneno ya Kiingereza yanayotumika katika nyanja hiyo yawe sasa yanatumika, bila ya kubadilishwa sana, katika lugha ya Kiswahili. Mifano iko mingi: folda (folder), kiibodi (keyboard), yuza nem (user name), kudelete (to delete), kusaaf au kubrauz (to surf, to browse), skrini (screen) na kontrol key (control key).

Jambo lililo muhimu ni kwamba tunapoanza kuyatumia maneno mepya yaliokubalika tuyatumie kwa njia ambayo itakuwa rahisi kwa msikilizaji au msomaji kuelewa unakusudia nini.

Maneno kama ‘tabia nchi’ na ‘utandawazi’ ingawa hayakuanza kutumika kwa muda mrefu sana hivi sasa yamekwishakuwa maneno ya kawaida yanayofahamika na wasikilizaji wa redio au televisheni au wasomaji wa magazeti na wa mablogi.

BBC Academy
http://www.bbc.co.uk/academy/swahili/language/new-words/article/art20131030124225972

Учебные тексты на суахили 2: Tafsiri nzuri na tafsiri mbovu

[Ёвин и Ива, не обращайте внимания. В Интернете не так просто найти хорошие тексты на суахили для учёбы, поэтому те, что мне попались, я буду складывать в блог]

Tafsiri ya neno kwa neno inadhoofisha maana – inaweza kupotosha maana ya kile kinachokusudiwa. Kwa hakika, kufasiri neno kwa neno huifanya tafsiri iwe mbovu.

Kila tafsiri ni fasiri au ufafanuzi wa maelezo fulani.

Sanaa ya kufasiri kwa Kiswahili si kazi rahisi kama wengi wanavyofikiri kwa sababu hakuna lugha iliyo sawa na Kiswahili.

Kazi ya kutafsiri maandishi kutoka lugha ya kigeni kwa Kiswahili inaweza kufanywa kwa urahisi na yeyote yule mwenye kamusi la maneno ya lugha hizo mbili.

Lakini fasiri yenye kutafsiri neno kwa neno sio tafsiri nzuri. Kwa hakika, si lazima kila neno lifasirike kwa neno moja. Maneno mengine huwa hayakubali kuamiliwa hivyo.

Mwenye kutafsiri anapoamua kutumia neno fulani badala ya jengine wakati huohuo anakuwa pia anachagua neno gani litalofuata ambalo atahitaji kulitumia.

Kwa hivyo uchaguzi wa neno ndio chanzo cha fasiri. Sauti pia, yaani namna neno linavyosikika husaidia kufikisha maana inayokusudiwa kwa wanaosikiliza au kusoma.

Tafsiri ya neno kwa neno inadhoofisha maana – inaweza kupotosha maana ya kile kinachokusudiwa. Kwa hakika, kufasiri neno kwa neno huifanya tafsiri iwe mbovu.

Tafsiri iliyo nzuri ni ile yenye kusema vilevile kama yasemavyo makala yaliyotafsiriwa, iwe inalingana na maandishi asili. Tafsiri iliyo nzuri huwa inaeleza mambo kana kwamba lugha iliyotumiwa ndio lugha asili iliyotumiwa kuandika makala hayo.

Tafsiri hiyo huwa na maana ya kinachokusudiwa katika maandishi yanayofasiriwa. Tafsiri aina hiyo huwa inatiririka kama maji; haikwami kwami.

Chaguo la neno moja linaweza kuamua mtiririko wa makala yote unayoyafasiri. Kutafsiri ni kazi ya hatua kwa hatua. Kwa hivyo, kumbuka kwamba unapoamua kutumia neno fulani katika hatua moja unaweza ukaiathiri hatua itayofuata hapo. Lakini kuchagua kutumia neno fulani na si jengine ni mwanzo tu.

Ni mwanzo kwa sababu tafsiri iliyo nzuri huwa pia inashikamana, sentensi moja inashikamana na nyingine, sehemu moja ya maelezo yanayofasiriwa inashikamana na nyingine.

Baadhi ya nyakati wafasiri wanaathiriwa na jinsi wafasiri wengine walivyotafsiri neno au mafungu ya maneno. Haya tunayaona wazi siku hizi katika matangazo ya redio au maandishi ya magazeti. Hatari hapa iko katika kuiga.

Kuna mifano mingi sana ya maneno yanayotafsiriwa vibaya na yanayoendelea kutumiwa na vyombo vya habari vya kuheshimika kwa sababu waandishi au watangazaji wamezoea kuigiza tafsiri zilizo mbovu.

Nitatoa hapa mifano miwili ya tafsiri mbovu. Zote zimetafsiri neno kwa neno na matokeo yake ni sentensi ambazo ingawa zina maneno ya Kiswahili hazisemi kama Waswahili tusemavyo.

1. “Waathiriwa wanapokea matibabu” ni tafsiri ya neno kwa neno ya sentensi ifuatayo ya Kiingereza: “The victims are receiving treatment.” Waswahili hatusemi kuwa “mgonjwa anapokea matibabu”. Tunasema kuwa “mgonjwa anatibiwa”.
2. “Je, unanipokea?” Hii ni tafsiri ya neno kwa neno ya sentensi ya Kiingereza: “Are you receiving me?” Mara nyingi tunawasikia watangazaji wakiisema sentensi hii wakiwa studio wakizungumza na ama waandishi wao au wahojiwa walio nje ya studio. Waswahili hatumuulizi mtu iwapo tunampokea. Tunamuuliza iwapo anatusikia. Lakini siku hizi kama nilivyosema watangazaji wamezoea kuwa “je, unanipokea?” badala ya “je, unasikia vizuri?”
Tafsiri nzuri haipatikani kwa uchawi. Inapatikana kwa juhudi za mwenye kufasiri za kuweza kuifanya tafsiri yake iwe na maana sawa na ile ya makala ya awali aliyoyafasiri.

Kuna jambo moja ambalo kila mwenye kufasiri anapaswa kulikumbuka. Nalo ni kwamba kazi ya kutafsiri kitu ni kazi ya usanii na si kazi ya sayansi. Hivyo, unaweza ukafasiri makala kwa uzuri utakiwavyo lakini bado anaweza akatokea mtu akaikosoa tafsiri yako.

Ni muhimu kwa hivyo kwamba usipoteze muda kubishana kuhusu, kwa mfano,namna ulivyozipanga sentensi zako. Lililo muhimu ambalo unapaswa ulizingatie ni iwapo tafsiri yako ina maana ileile kama iliyokusudiwa katika makala ya Kiingereza (au ya lugha yoyote nyingine) uliyoyafasiri.

Unapofasiri kitu usiwe na papara. Kuna hatari kwamba ukifanya pupa unaweza ukapotosha maana ya kinachokusudiwa. Soma kwa makini, mara mbili tatu ikiwezekana, hicho unachokitafsiri mpaka maana yake ikuingie sawasawa kichwani. Usianze kutafsiri chochote kabla ya kwanza kukielewa unachokifasiri. Halafu unapokuwa unafasiri ziangalie sentensi zako, au hata zisome kwa sauti, uangalie kama zinalingana na miundo ya sentensi za Kiswahili.

Jiulize pia iwapo fasiri yako ni sahihi na iwapo inafahamika vizuri. Haitoweza kufahamika iwapo utatumia miundo ya sentensi yenye kuigiza ile ya lugha ya Kiingereza (au lugha yoyote nyingine ya awali unayoifasiri).

Pia tafsiri yako haitoweza kufahamika ikiwa makala unayoyafasiri hayafahamiki. Kwa hivyo, usichelee kuwauliza wengine maana ya unachotaka kukitafsiri. Waombe wenzako wakueleze makala uliyo nayo yana maana gani au yanasema nini.

Tunapotafsiri huwa hatufasiri maneno tu bali huwa pia tunafasiri ada, kawaida, na utamaduni wa mila na hata wa kisiasa. Tunakuwa tunazishughulikia lugha mbili tafauti — au pingine zaidi ya mbili — na wakati huohuo tunakuwa pia tunashughulikia tamaduni mbili tafauti.

Kwa hivyo, jiepushe kutumia mifano kutoka tamaduni nyingine, jaribu uwezavyo kutumia mifano kutoka kwenye utamaduni wa Kiswahili.

Kwa hakika, inaweza kuwa kazi ngumu kutafsiri maneno ya kitamaduni. Tafauti baina ya tamaduni mbalimbali ni changamoto kubwa kwani tafauti hizo huenda zikampa matatizo mwenye kutafsiri kuliko tafauti za miundo ya lugha.

Kwa mfano, katika lugha yetu ya Kiswahili kuna maneno ambayo hatuyasemi waziwazi. Sehemu za utupu wa mwanadamu hatuziiti kwa majina yao. Ni muhali Waswahili kuziita sehemu hizo za utupu kwa majina yao. Lakini Waingereza hawana muhali huo. Wanayatumia katika mazungumzo na maandishi ya kawaida.

Hamna shaka yoyote ile kwamba kuyatafsiri maneno kama hayo kwa Kiswahili huwa ni kazi ngumu na huwatatiza baadhi ya wanaotafsiri.

Ugumu huo huenda ukawa ni kwa sababu ya tafauti baina ya tamaduni, dini, au imani. Kuna njia mbalimbali za kutafsiri maneno yenye muhali kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Tafsiri nzuri ni ile iliyo tiifu kwa makala ya chanzo, makala ya awali na pia inayowafanya watu wanaoisikiliza au kuisoma waikubali kwa namna makala yalivyotafsiriwa.

Tafauti baina ya tamaduni mbili zinaweza kuwafanya watu wa utamaduni mmoja waamini mambo, matukio au hata tabia ambazo watu wa utamaduni mwingine huenda wakaziona kuwa ni za ajabuajabu au za kuchekesha au hata zisizokubalika katika utamaduni wao.

Kila wakati mtafsiri anawajibika amfikiriye msikilizaji au msomaji wa makala au taarifa iliyotafsiriwa.

Kwa mfano ikiwa umetafsiri makala yatayotumiwa katika kipindi cha watoto cha redio au cha televisheni basi utalazimika uwe mwangalifu zaidi wa lugha utayoitumia ambayo itabidi iwe nyepesi.

BBC Academy
http://www.bbc.co.uk/academy/swahili/language/translation/article/art20131011115926129

Учебные тексты на суахили 1: Nini kitafanyika sasa baada ya uchaguzi Uingereza?

[Ёвин и Ива, не обращайте внимания. В Интернете не так просто найти хорошие тексты на суахили для учёбы, поэтому те, что мне попались, я буду складывать в блог]

Nini hufanyika kukikosekana mshindi wa moja kwa moja katika uchaguzi mkuu?
Chama chenye wabunge wengi ndicho pekee huunda serikali?

Si lazima. Chama chenye wabunge wengi baada ya kura zote kuhesabiwa maeneo yote 650, huwa kinatangazwa mshindi na kiongozi wake huwa waziri mkuu. Lakini hili huenda lisifanyike wakati huu kwa kuwa chama kilichoshinda hakina wingi wa wabunge. Inawezekana kwa chama kilichomaliza cha pili kuunda serikali.

Mtu hushinda vipi uchaguzi?
Njia rahisi zaidi kwa mtu kuwa waziri mkuu ni chama chake kupata wingi wa wabunge katika Bunge la Commons – kuwa na wabunge wengi kuliko wabunge wote wa vyama hivyo vingine wakijumlishwa.

Unahitaji wabunge wangapi kuwa na wingi?
Idadi ya wabunge wanaohitajika ni 326. Wabunge hao watatosha kupitisha sheria mpya bila kushindwa na upinzani. Hilo likikosekana, huwa kuna bunge la mng’ang’anio.

Bunge la mng’ang’anio ni gani?
Ni wakati ambapo hakuna chaka hata kimoja kinachoweza kuwa na wingi wa wabunge kivyake. Hilo lilifanyika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kutatokea nini kukiwa na Bunge la mng’ang’anio tena?
Kutakuwa na msururu wa mashauriano kati ya viongozi wa vyama na wajumbe wao, wakijaribu kuunda serikali ya muungano au muungano wa kushindwa, kujaribu kusaidia kiongozi wa Conservative Theresa May au kiongozi wa Labour Jeremy Corbyn (watu wawili pekee kwa sasa walio na nafasi nzuri ya kuunda serikali) kuunda serikali.
Mmoja kati ya wawili hao anaweza pia kuamua kusimama kivyake na kujaribu kuunda serikali ya wachache, kwa kutegemea vyama vidogo anapohitaji kupitisha sheria mpya.

Nani atapata nafasi ya kwanza kuunda muungano?
Theresa May ataendelea kuwa waziri mkuu akiendelea kujaribu kuunda muungano wenyewe wabunge wengi.
Ikibainika kwamba hawezi, na Jeremy Corbyn anaweza, basi May atatakiwa kujiuzulu. Bw Corbyn naye atakuwa waziri mkuu wakati huo.
Lakini si lazima Corbyn asubiri hadi May amalize njia zake zote za kujaribu kuunda muungano kabla yake kuanza juhudi zake. Anaweza kushauriana na washirika watarajiwa wakati May naye akiendelea na mashauriano yake. Unaweza hata kupata wote wawili wanashauriana na vyama au viongozi sawa.

Hii itachukua muda gani?
Hakuna muda rasmi. Ilichukua siku tano mwaka 2010 kuunda muungano, lakini kawaida huchukua muda mrefu kuliko hivyo.

Mashauriano yanaweza kuendelea milele?
Kwa sasa, muda wa mwisho wa kwanza ni Jumanne tarehe 13 Bunge litakapokutana mara ya kwanza. Bi May ana hadi wakati huo kuunda muungano wa kumuwezesha kusalia madarakani au ajiuzulu, kwa mujibu wa mwongozo kutoka kwa afisi ya Baraza la Mawaziri.
Lakini Bi May lazima awe anafahamu kwamba Jeremy Corbyn anaweza kuunda serikali lakini yeye hawezi.

Na ikitokea iwe kwamba haibainiki iwapo serikali mpya inaweza kuundwa?
Njia pekee ya kufahamu iwapo serikali inaweza kuundwa ni iwapo ina imani na Bunge la Commons. Maana yake ni kwamba, je, serikali inaweza kupitisha sheria mpya zilizopendekezwa kwenye Hotuba ya Malkia? Hotuba ya Malkia inapangiwa kutolewa Jumatatu 19 Juni.
Theresa May anaweza kuamua kusalia na kubahatisha kuona iwapo anaweza kupata kura za kutosha kutoka kwa vyama vingine kupitisha sheria hizo.
Iwapo atakuwa amejiuzulu wakati huo na kumkabidhi Bw Corbyn nafasi, basi utakuwa mtihani kwa kiongozi huyo wa Labour kuonesha iwapo anaweza kuunda serikali.
Iwapo SNP watapata viti ambavyo wamebashiriwa kupata, wanaweza kutekeleza jukumu muhimu.
Msimamo wao umekuwa kwamba hawataunga mkono serikali ya Conservative.

Malkia hutekeleza wajibu gani?
Kiongozi wa chama anayeweza kumwambia Malkia kwamba ana idadi ya wabunge wa kutosha kuunda serikali ndiye atakayepewa idhini na Malkia kuunda serikali.
Malkia huwa hajihusishi na siasa, hivyo hakuna vile anavyoweza kumchagua waziri mkuu.
Kumekuwa na mapendekezo kwamba huenda Malkia akakosa kuwasilisha hotuba yake yeye binafsi iwapo kutakuwa na shaka kwamba huenda ikakosa kupitishwa.

Muungano ni nini?
Serikali ya Muungano huwa ni wakati vyama viwili ama zaidi vinashirikiana kuunda serikali moja. Washirika wenye wabunge wachache hugawiwa nyadhifa za mawaziri na pia mpango mmoja wa serikali hutayarishwa.

Serikali ya wachache huwa ni gani?
Chama cha Conservatives au cha Labour kikashindwa kuunda muungano au kujisimamia kivyake kuunda serikali, kinaweza kuunda serikali ya wachache na kuteua mawaziri wake.
Chama hicho hakiwezi kupitisha sheria bila kura kutoka vyama vingine ambavyo havimo serikalini.
Mfano, Labour wanaweza kuunda serikali ya wachache ikiongoziwa na Jeremy Corbyn kama Waziri Mkuu, lakini chama hicho kitahitaji kura kutoka vyama vya Scottish National Party (SNP) na Liberal Democrat kupitisha sheria bungeni.

Chama kinachomaliza cha pili hivyo kinaweza kuunda serikali?
Ndio. Iwapo kuna shaka iwapo umma unaweza kuikubali serikali hiyo.

Kutakuwa na uchaguzi mpya?
Awali, kunapoundwa serikali ya wachache, waziri mkuu baadaye huitisha uchaguzi mwingine nafasi nzuri inapojitokeza na kujaribu kupata wingi wa wabunge. Au, upinzani hushurutisha kufanyike uchaguzi mwingine kwa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na serikali.
Ndipo uchaguzi mpya ufanyike hata hivyo itahitaji:
– Theluthi mbili ya wabunge waunge mkono pendekezo la kuandaa uchaguzi. Hii in maana kwamba itabidi Labour na Conservative waunge mkono.
– Kura ya kutokuwa na imani na serikali ipitishwe na wabunge wengi. Uchaguzi unaweza kufanyika katika chini ya siku 14 baada ya hapo serikali isipofanikiwa kushinda kura ya kutokuwa na imani nayo kabla ya muda huo kumalizika.

BBC Swahili, 9 Juni 2017
http://www.bbc.com/swahili/habari-40208610