Учебные тексты на суахили 2: Tafsiri nzuri na tafsiri mbovu

[Ёвин и Ива, не обращайте внимания. В Интернете не так просто найти хорошие тексты на суахили для учёбы, поэтому те, что мне попались, я буду складывать в блог]

Tafsiri ya neno kwa neno inadhoofisha maana – inaweza kupotosha maana ya kile kinachokusudiwa. Kwa hakika, kufasiri neno kwa neno huifanya tafsiri iwe mbovu.

Kila tafsiri ni fasiri au ufafanuzi wa maelezo fulani.

Sanaa ya kufasiri kwa Kiswahili si kazi rahisi kama wengi wanavyofikiri kwa sababu hakuna lugha iliyo sawa na Kiswahili.

Kazi ya kutafsiri maandishi kutoka lugha ya kigeni kwa Kiswahili inaweza kufanywa kwa urahisi na yeyote yule mwenye kamusi la maneno ya lugha hizo mbili.

Lakini fasiri yenye kutafsiri neno kwa neno sio tafsiri nzuri. Kwa hakika, si lazima kila neno lifasirike kwa neno moja. Maneno mengine huwa hayakubali kuamiliwa hivyo.

Mwenye kutafsiri anapoamua kutumia neno fulani badala ya jengine wakati huohuo anakuwa pia anachagua neno gani litalofuata ambalo atahitaji kulitumia.

Kwa hivyo uchaguzi wa neno ndio chanzo cha fasiri. Sauti pia, yaani namna neno linavyosikika husaidia kufikisha maana inayokusudiwa kwa wanaosikiliza au kusoma.

Tafsiri ya neno kwa neno inadhoofisha maana – inaweza kupotosha maana ya kile kinachokusudiwa. Kwa hakika, kufasiri neno kwa neno huifanya tafsiri iwe mbovu.

Tafsiri iliyo nzuri ni ile yenye kusema vilevile kama yasemavyo makala yaliyotafsiriwa, iwe inalingana na maandishi asili. Tafsiri iliyo nzuri huwa inaeleza mambo kana kwamba lugha iliyotumiwa ndio lugha asili iliyotumiwa kuandika makala hayo.

Tafsiri hiyo huwa na maana ya kinachokusudiwa katika maandishi yanayofasiriwa. Tafsiri aina hiyo huwa inatiririka kama maji; haikwami kwami.

Chaguo la neno moja linaweza kuamua mtiririko wa makala yote unayoyafasiri. Kutafsiri ni kazi ya hatua kwa hatua. Kwa hivyo, kumbuka kwamba unapoamua kutumia neno fulani katika hatua moja unaweza ukaiathiri hatua itayofuata hapo. Lakini kuchagua kutumia neno fulani na si jengine ni mwanzo tu.

Ni mwanzo kwa sababu tafsiri iliyo nzuri huwa pia inashikamana, sentensi moja inashikamana na nyingine, sehemu moja ya maelezo yanayofasiriwa inashikamana na nyingine.

Baadhi ya nyakati wafasiri wanaathiriwa na jinsi wafasiri wengine walivyotafsiri neno au mafungu ya maneno. Haya tunayaona wazi siku hizi katika matangazo ya redio au maandishi ya magazeti. Hatari hapa iko katika kuiga.

Kuna mifano mingi sana ya maneno yanayotafsiriwa vibaya na yanayoendelea kutumiwa na vyombo vya habari vya kuheshimika kwa sababu waandishi au watangazaji wamezoea kuigiza tafsiri zilizo mbovu.

Nitatoa hapa mifano miwili ya tafsiri mbovu. Zote zimetafsiri neno kwa neno na matokeo yake ni sentensi ambazo ingawa zina maneno ya Kiswahili hazisemi kama Waswahili tusemavyo.

1. “Waathiriwa wanapokea matibabu” ni tafsiri ya neno kwa neno ya sentensi ifuatayo ya Kiingereza: “The victims are receiving treatment.” Waswahili hatusemi kuwa “mgonjwa anapokea matibabu”. Tunasema kuwa “mgonjwa anatibiwa”.
2. “Je, unanipokea?” Hii ni tafsiri ya neno kwa neno ya sentensi ya Kiingereza: “Are you receiving me?” Mara nyingi tunawasikia watangazaji wakiisema sentensi hii wakiwa studio wakizungumza na ama waandishi wao au wahojiwa walio nje ya studio. Waswahili hatumuulizi mtu iwapo tunampokea. Tunamuuliza iwapo anatusikia. Lakini siku hizi kama nilivyosema watangazaji wamezoea kuwa “je, unanipokea?” badala ya “je, unasikia vizuri?”
Tafsiri nzuri haipatikani kwa uchawi. Inapatikana kwa juhudi za mwenye kufasiri za kuweza kuifanya tafsiri yake iwe na maana sawa na ile ya makala ya awali aliyoyafasiri.

Kuna jambo moja ambalo kila mwenye kufasiri anapaswa kulikumbuka. Nalo ni kwamba kazi ya kutafsiri kitu ni kazi ya usanii na si kazi ya sayansi. Hivyo, unaweza ukafasiri makala kwa uzuri utakiwavyo lakini bado anaweza akatokea mtu akaikosoa tafsiri yako.

Ni muhimu kwa hivyo kwamba usipoteze muda kubishana kuhusu, kwa mfano,namna ulivyozipanga sentensi zako. Lililo muhimu ambalo unapaswa ulizingatie ni iwapo tafsiri yako ina maana ileile kama iliyokusudiwa katika makala ya Kiingereza (au ya lugha yoyote nyingine) uliyoyafasiri.

Unapofasiri kitu usiwe na papara. Kuna hatari kwamba ukifanya pupa unaweza ukapotosha maana ya kinachokusudiwa. Soma kwa makini, mara mbili tatu ikiwezekana, hicho unachokitafsiri mpaka maana yake ikuingie sawasawa kichwani. Usianze kutafsiri chochote kabla ya kwanza kukielewa unachokifasiri. Halafu unapokuwa unafasiri ziangalie sentensi zako, au hata zisome kwa sauti, uangalie kama zinalingana na miundo ya sentensi za Kiswahili.

Jiulize pia iwapo fasiri yako ni sahihi na iwapo inafahamika vizuri. Haitoweza kufahamika iwapo utatumia miundo ya sentensi yenye kuigiza ile ya lugha ya Kiingereza (au lugha yoyote nyingine ya awali unayoifasiri).

Pia tafsiri yako haitoweza kufahamika ikiwa makala unayoyafasiri hayafahamiki. Kwa hivyo, usichelee kuwauliza wengine maana ya unachotaka kukitafsiri. Waombe wenzako wakueleze makala uliyo nayo yana maana gani au yanasema nini.

Tunapotafsiri huwa hatufasiri maneno tu bali huwa pia tunafasiri ada, kawaida, na utamaduni wa mila na hata wa kisiasa. Tunakuwa tunazishughulikia lugha mbili tafauti — au pingine zaidi ya mbili — na wakati huohuo tunakuwa pia tunashughulikia tamaduni mbili tafauti.

Kwa hivyo, jiepushe kutumia mifano kutoka tamaduni nyingine, jaribu uwezavyo kutumia mifano kutoka kwenye utamaduni wa Kiswahili.

Kwa hakika, inaweza kuwa kazi ngumu kutafsiri maneno ya kitamaduni. Tafauti baina ya tamaduni mbalimbali ni changamoto kubwa kwani tafauti hizo huenda zikampa matatizo mwenye kutafsiri kuliko tafauti za miundo ya lugha.

Kwa mfano, katika lugha yetu ya Kiswahili kuna maneno ambayo hatuyasemi waziwazi. Sehemu za utupu wa mwanadamu hatuziiti kwa majina yao. Ni muhali Waswahili kuziita sehemu hizo za utupu kwa majina yao. Lakini Waingereza hawana muhali huo. Wanayatumia katika mazungumzo na maandishi ya kawaida.

Hamna shaka yoyote ile kwamba kuyatafsiri maneno kama hayo kwa Kiswahili huwa ni kazi ngumu na huwatatiza baadhi ya wanaotafsiri.

Ugumu huo huenda ukawa ni kwa sababu ya tafauti baina ya tamaduni, dini, au imani. Kuna njia mbalimbali za kutafsiri maneno yenye muhali kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Tafsiri nzuri ni ile iliyo tiifu kwa makala ya chanzo, makala ya awali na pia inayowafanya watu wanaoisikiliza au kuisoma waikubali kwa namna makala yalivyotafsiriwa.

Tafauti baina ya tamaduni mbili zinaweza kuwafanya watu wa utamaduni mmoja waamini mambo, matukio au hata tabia ambazo watu wa utamaduni mwingine huenda wakaziona kuwa ni za ajabuajabu au za kuchekesha au hata zisizokubalika katika utamaduni wao.

Kila wakati mtafsiri anawajibika amfikiriye msikilizaji au msomaji wa makala au taarifa iliyotafsiriwa.

Kwa mfano ikiwa umetafsiri makala yatayotumiwa katika kipindi cha watoto cha redio au cha televisheni basi utalazimika uwe mwangalifu zaidi wa lugha utayoitumia ambayo itabidi iwe nyepesi.

BBC Academy
http://www.bbc.co.uk/academy/swahili/language/translation/article/art20131011115926129

Учебные тексты на суахили 1: Nini kitafanyika sasa baada ya uchaguzi Uingereza?

[Ёвин и Ива, не обращайте внимания. В Интернете не так просто найти хорошие тексты на суахили для учёбы, поэтому те, что мне попались, я буду складывать в блог]

Nini hufanyika kukikosekana mshindi wa moja kwa moja katika uchaguzi mkuu?
Chama chenye wabunge wengi ndicho pekee huunda serikali?

Si lazima. Chama chenye wabunge wengi baada ya kura zote kuhesabiwa maeneo yote 650, huwa kinatangazwa mshindi na kiongozi wake huwa waziri mkuu. Lakini hili huenda lisifanyike wakati huu kwa kuwa chama kilichoshinda hakina wingi wa wabunge. Inawezekana kwa chama kilichomaliza cha pili kuunda serikali.

Mtu hushinda vipi uchaguzi?
Njia rahisi zaidi kwa mtu kuwa waziri mkuu ni chama chake kupata wingi wa wabunge katika Bunge la Commons – kuwa na wabunge wengi kuliko wabunge wote wa vyama hivyo vingine wakijumlishwa.

Unahitaji wabunge wangapi kuwa na wingi?
Idadi ya wabunge wanaohitajika ni 326. Wabunge hao watatosha kupitisha sheria mpya bila kushindwa na upinzani. Hilo likikosekana, huwa kuna bunge la mng’ang’anio.

Bunge la mng’ang’anio ni gani?
Ni wakati ambapo hakuna chaka hata kimoja kinachoweza kuwa na wingi wa wabunge kivyake. Hilo lilifanyika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kutatokea nini kukiwa na Bunge la mng’ang’anio tena?
Kutakuwa na msururu wa mashauriano kati ya viongozi wa vyama na wajumbe wao, wakijaribu kuunda serikali ya muungano au muungano wa kushindwa, kujaribu kusaidia kiongozi wa Conservative Theresa May au kiongozi wa Labour Jeremy Corbyn (watu wawili pekee kwa sasa walio na nafasi nzuri ya kuunda serikali) kuunda serikali.
Mmoja kati ya wawili hao anaweza pia kuamua kusimama kivyake na kujaribu kuunda serikali ya wachache, kwa kutegemea vyama vidogo anapohitaji kupitisha sheria mpya.

Nani atapata nafasi ya kwanza kuunda muungano?
Theresa May ataendelea kuwa waziri mkuu akiendelea kujaribu kuunda muungano wenyewe wabunge wengi.
Ikibainika kwamba hawezi, na Jeremy Corbyn anaweza, basi May atatakiwa kujiuzulu. Bw Corbyn naye atakuwa waziri mkuu wakati huo.
Lakini si lazima Corbyn asubiri hadi May amalize njia zake zote za kujaribu kuunda muungano kabla yake kuanza juhudi zake. Anaweza kushauriana na washirika watarajiwa wakati May naye akiendelea na mashauriano yake. Unaweza hata kupata wote wawili wanashauriana na vyama au viongozi sawa.

Hii itachukua muda gani?
Hakuna muda rasmi. Ilichukua siku tano mwaka 2010 kuunda muungano, lakini kawaida huchukua muda mrefu kuliko hivyo.

Mashauriano yanaweza kuendelea milele?
Kwa sasa, muda wa mwisho wa kwanza ni Jumanne tarehe 13 Bunge litakapokutana mara ya kwanza. Bi May ana hadi wakati huo kuunda muungano wa kumuwezesha kusalia madarakani au ajiuzulu, kwa mujibu wa mwongozo kutoka kwa afisi ya Baraza la Mawaziri.
Lakini Bi May lazima awe anafahamu kwamba Jeremy Corbyn anaweza kuunda serikali lakini yeye hawezi.

Na ikitokea iwe kwamba haibainiki iwapo serikali mpya inaweza kuundwa?
Njia pekee ya kufahamu iwapo serikali inaweza kuundwa ni iwapo ina imani na Bunge la Commons. Maana yake ni kwamba, je, serikali inaweza kupitisha sheria mpya zilizopendekezwa kwenye Hotuba ya Malkia? Hotuba ya Malkia inapangiwa kutolewa Jumatatu 19 Juni.
Theresa May anaweza kuamua kusalia na kubahatisha kuona iwapo anaweza kupata kura za kutosha kutoka kwa vyama vingine kupitisha sheria hizo.
Iwapo atakuwa amejiuzulu wakati huo na kumkabidhi Bw Corbyn nafasi, basi utakuwa mtihani kwa kiongozi huyo wa Labour kuonesha iwapo anaweza kuunda serikali.
Iwapo SNP watapata viti ambavyo wamebashiriwa kupata, wanaweza kutekeleza jukumu muhimu.
Msimamo wao umekuwa kwamba hawataunga mkono serikali ya Conservative.

Malkia hutekeleza wajibu gani?
Kiongozi wa chama anayeweza kumwambia Malkia kwamba ana idadi ya wabunge wa kutosha kuunda serikali ndiye atakayepewa idhini na Malkia kuunda serikali.
Malkia huwa hajihusishi na siasa, hivyo hakuna vile anavyoweza kumchagua waziri mkuu.
Kumekuwa na mapendekezo kwamba huenda Malkia akakosa kuwasilisha hotuba yake yeye binafsi iwapo kutakuwa na shaka kwamba huenda ikakosa kupitishwa.

Muungano ni nini?
Serikali ya Muungano huwa ni wakati vyama viwili ama zaidi vinashirikiana kuunda serikali moja. Washirika wenye wabunge wachache hugawiwa nyadhifa za mawaziri na pia mpango mmoja wa serikali hutayarishwa.

Serikali ya wachache huwa ni gani?
Chama cha Conservatives au cha Labour kikashindwa kuunda muungano au kujisimamia kivyake kuunda serikali, kinaweza kuunda serikali ya wachache na kuteua mawaziri wake.
Chama hicho hakiwezi kupitisha sheria bila kura kutoka vyama vingine ambavyo havimo serikalini.
Mfano, Labour wanaweza kuunda serikali ya wachache ikiongoziwa na Jeremy Corbyn kama Waziri Mkuu, lakini chama hicho kitahitaji kura kutoka vyama vya Scottish National Party (SNP) na Liberal Democrat kupitisha sheria bungeni.

Chama kinachomaliza cha pili hivyo kinaweza kuunda serikali?
Ndio. Iwapo kuna shaka iwapo umma unaweza kuikubali serikali hiyo.

Kutakuwa na uchaguzi mpya?
Awali, kunapoundwa serikali ya wachache, waziri mkuu baadaye huitisha uchaguzi mwingine nafasi nzuri inapojitokeza na kujaribu kupata wingi wa wabunge. Au, upinzani hushurutisha kufanyike uchaguzi mwingine kwa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na serikali.
Ndipo uchaguzi mpya ufanyike hata hivyo itahitaji:
– Theluthi mbili ya wabunge waunge mkono pendekezo la kuandaa uchaguzi. Hii in maana kwamba itabidi Labour na Conservative waunge mkono.
– Kura ya kutokuwa na imani na serikali ipitishwe na wabunge wengi. Uchaguzi unaweza kufanyika katika chini ya siku 14 baada ya hapo serikali isipofanikiwa kushinda kura ya kutokuwa na imani nayo kabla ya muda huo kumalizika.

BBC Swahili, 9 Juni 2017
http://www.bbc.com/swahili/habari-40208610